RAIS MWINYI:TUTANGAZE SERA ZA VYAMA NA SI KUENEZA CHUKI KWA WANANCHI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewasihi wanasiasa kutumia majukwaa ya kisiasa kutangaza sera za vyama vyao kwa wananchi badala ya kueneza siasa za chuki.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipotoa salamu kwa waumini wa dini ya Kiislamu baada ya Sala ya Ijumaa na dua maalum ya kuwaombea viongozi wakuu wa nchi, iliyofanyika katika Msikiti wa Shaafi, Mbuyu Mnene, Mkoa wa Mjini Magharibi leo tarehe 15 Agosti, 2025.



Amesema ni vema wanasiasa kuhubiri amani na kueleza namna watakavyowatumikia wananchi baada ya kupata ridhaa ya kuwaongoza, badala ya kutangaza siasa za chuki, matusi na mifarakano ndani ya jamii.



Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amewasisitiza viongozi wa dini na waumini kuiombea nchi amani hasa katika kipindi hiki ambacho kimebakia miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu. Amesema bila amani hakuna jambo lolote la maendeleo linaloweza kufanikishwa.




Kwa upande mwingine, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa kila raia mwema ana wajibu wa kuhakikisha amani ya nchi inadumu wakati wote.

Share: