
BBC imefichua mtandao wa biashara ya ngono unaodaiwa kuendeshwa na raia wa Uganda anayeishi Dubai, Charles Mwesigwa. Upelelezi wa siri umeonesha kuwa wanawake wachanga, hasa kutoka Uganda, wanadanganywa kwa ahadi za kazi halali katika maduka na hoteli za Uarabuni, lakini wanapowasili Dubai hujikuta wakisukumwa katika biashara ya ngono.
Tahadhari: Ripoti hii inahusu visa vya unyanyasaji wa kingono
Mwesigwa, ambaye anasema aliwahi kuwa dereva wa basi jijini London, alinaswa akieleza kwamba anaweza kupanga wanawake kwa wateja matajiri kuanzia dola 1,000 kwa usiku mmoja. Aidha, alisema wanawake hao "wanaweza kufanya karibu kila kitu," ikiwemo matendo yasiyo ya kawaida ya kingono.
Mojawapo ya waathiriwa, aliyepewa jina la kubuni Mia, alieleza kuwa alilazimishwa kulipa deni la zaidi ya paundi 2,000 lililodaiwa kuwa gharama ya tiketi na makazi, na deni hilo liliendelea kuongezeka kila wiki. Alidai wateja wengi walikuwa raia wa Ulaya wenye maombi ya kinyama ya kingono. Mwanamke mwingine, Lexi, alithibitisha simulizi hizo, akiongeza kuwa mara nyingi walilazimishwa kushiriki vitendo vya unyanyasaji vikubwa kwa malipo.
Lexi alisema alijaribu kupata msaada wa polisi wa Dubai, lakini alikataliwa kwa misingi ya kibaguzi. Hatimaye aliweza kutoroka na kurudi Uganda, ambako sasa anasaidia wanawake wengine waliokwama katika mazingira hayo.
BBC imebaini kuwa angalau wanawake wawili wanaohusishwa na Mwesigwa walifariki dunia kwa kuruka kutoka majengo marefu. Miongoni mwao ni Monic Karungi na Kayla Birungi. Ingawa vifo vyao vilihukumiwa kama kujiua, familia na marafiki wamesema uchunguzi haukufanywa ipasavyo.
Monic, ambaye alihadaiwa kwenda kufanya kazi ya duka, alidaiwa kudaiwa zaidi ya dola 27,000 na alikuwa akijaribu kuondoka kwenye mtandao huo kabla ya kifo chake mwaka 2022. Mwili wake ulizikwa katika makaburi ya “The Unknown” mjini Dubai, badala ya kurejeshwa nyumbani Uganda.
Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa na BBC, Mwesigwa alionekana kuendesha mtandao wake kwa kuwatumia watu wengine kusajili mali na magari, ili jina lake lisihusishwe moja kwa moja. Mashahidi waliodai kumfahamu walisema wanawake wake walipelekwa kwenye vilabu na sherehe za kifahari ili kuwapata wateja – ikiwemo wachezaji wa soka, wanamuziki, na hata viongozi wa kisiasa.
Alipoulizwa na BBC, Mwesigwa alikanusha mashtaka yote, akidai yeye ni “mtu wa sherehe” tu na kwamba wasichana wanamfuata kwa sababu ya uhusiano wake na watu matajiri. Hata hivyo, hakutoa maelezo kuhusu vifo vya wanawake wawili waliopoteza maisha wakiwa na uhusiano naye. Polisi wa Dubai hawakujibu maombi ya BBC kupata rekodi za uchunguzi wa matukio hayo.
Mashirika ya kijamii nchini Uganda yameonya kuwa tatizo la vijana kupelekwa Ghuba kwa ahadi za ajira linaweka maisha ya wengi hatarini. Wanasema baadhi ya wasichana huishia kuuzwa kwenye mtandao wa ngono badala ya kupata ajira walizoahidiwa.
Familia za wahanga sasa zinataka uchunguzi wa kina na hatua kali zichukuliwe ili kuzuia visa kama hivi kuendelea. Kama alivyoeleza ndugu wa Monic:
“Sote tunaangalia kifo cha Monic, lakini nani anawaangalia wasichana ambao bado wako hai?”
Chanzo: BBC