
Mvutano mkali umeibuka kati ya Diamond Platnumz, na aliyekuwa msanii wake, Mbosso, kufuatia mfululizo wa jumbe za kukinzana zilizozima shughuli zote kwenye kiwanda cha muziki.
Sakata hilo lilianza kwa Mbosso kumtaka Diamond amkanye Baba Levo kuongea kauli za kumkwaza. Diamond alijibu na kumtaka Mbosso asijihusishe na "ujinga" unaoendelea. Kisha, akifichua mengi, Diamond alidai kuwa alimkopesha Mbosso kiasi cha Shilingi milioni 323, ambacho alimsamehe kama mchango wake wa kumsaidia Mbosso kuanza maisha baada ya kuondoka Wasafi.
Pia, Diamond alisisitiza kuwa hata wimbo wa "Pawa" aliufanyia kazi yeye na kuusaidia kuwa maarufu. Akijitetea dhidi ya madai ya wivu, Diamond alisema hawezi kumonea gere kwa EP au wimbo mmoja wakati yeye ana mafanikio makubwa zaidi.
Mbosso ameandika akijibu kwa unyenyekevu, akikanusha kuwa hajawahi kusema kwamba Diamond anamuonea wivu na badala yake, alimtaka Diamond asome andiko lakea mwanzo "kwa utulivu bila kupanic". Mbosso alionyesha shukrani zake za dhati, akisema mchango wa Diamond kwenye maisha yake ni mkubwa kiasi kwamba hata Mwenyezi Mungu hawezi kumbariki akimkosea. Alisisitiza kuwa "Hizi kauli za Wiyu zinazojijenga kwako ni Nguvu ya Shetani anayetaka kukufanya unichukie".
Licha ya majibu ya upatanishi, Diamond alimaliza mfululizo wa jumbe zake kwa kusema ameamua kukubali jukumu la kuwa "mtu mbaya" na kuachia wengine washinde, ingawa alitoa onyo kuwa endapo atachokozwa tena, anaweza kufichua mambo ambayo hayatawapendeza.